Kwa miongo mingi, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa likitoa matamko mara kwa mara kulaani janga la unyanyasaji wa kijinsia ambalo linaendelea kushuhudiwa duniani kote.  Hivi karibuni, kamati kuu ya WCC ilisema:

“Tunatambua kuwa unyanyasaji wa kingono na wa kijinsia ni dhahiri katika mazingira mengi tofauti na mara nyingi yaliyofichika... hatari na athari zake ni... mwiko katika makanisa mengi na jumuiya za kanisa, kuzuia kanisa kuwa mahali salama na penye ulinzi kwa wanawake ambao ni waathiriwa wa unyanyasaji au wanaotishiwa na Ukatili wa Kingono na Kijinsia. Kanisa lazima lichangie kikamilifu katika kuondoa ukatili na unyanyasaji huo.”[1]

Tangu mwaka 2011 WCC iliposhughulikia hadharani unyanyasaji wa kingono uliofanywa na makasisi, [2] visa vya unyanyasaji wa kingono katika miktadha ya kanisa, zamani na sasa, vinazidi kuripotiwa. Kadiri viongozi wa kanisa wanavyoendelea kutajwa katika visa vya ukatili wa kingono, visa hivi vinawataka viongozi wa kanisa kukiri uhusika wao katika kuendeleza tatizo na kuwalinda wanyanyasaji bila kujali ustawi wa kiakili, kihisia, kimwili na kiroho wa aliyenyanyaswa.

Tunalalamika kwamba unyonyaji wa kingono, ukatili na unyanyasaji unatokana na kutengwa kwa wanawake, watoto na watu wengine walio katika mazingira hatarishi. Tunasikitika kwamba suala hili linatokea katika sekta zote na katika ngazi zote katika jamii yetu, pamoja na katika jamii za kanisa, na kwa viongozi waliokabidhiwa na jamii zao wawahudumie na kuwatunza wote, hasa wale walio katika mazingira hatarishi. Dhambi ya ukatili inajumuishwa mara nyingi sana na kushindwa kwa wafanyakazi wa kanisa, miundo na mifumo ya kiutendaji, kwa maneno na vitendo ambavyo vinamlaumu mtu aliyefanyiwa ukatili, na kwa ukimya unaokataa haki yoyote. Wakati mwingine, kushindwa kwetu kwa pamoja kuyapa kipaumbele matukio yaliyoripotiwa kumeficha ukweli na kuwanyamazisha wanaonyanyaswa, na hivyo kumlinda mnyanyasaji.

Kukubali na kutubu vitendo vya ukatili na unyanyasaji ni muhimu. Lakini lazima tufuatilie hatua inayopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha theolojia yetu, elimu yetu, miundo yetu, uongozi wetu, na utawala wetu unazuia ukatili na unyanyasaji kama huo. Kila ripoti au madai ya unyanyasaji wa kijinsia lazima yachukuliwe kwa uzito mkubwa na kuchunguzwa kwa uhuru, bila upendeleo na kwa kina. Wahusika wote katika uchunguzi wanapaswa kusaidiwa vizuri katika mchakato wote ikiwa ni pamoja na kupewa huduma ya kichungaji, haki ya kiutaratibu na haki ya asili. Ambapo uchunguzi unahitimisha kuwa unyanyasaji umetokea mwathiriwa lazima apate usaidizi bora kabisa na kufidiwa vizuri kabisa kadiri iwezekanavyo na mhalifu awajibishwe.

Tunafanya upya ahadi yetu ya kuzuia aina zote za vitendo viovu, hasa unyonyaji na unyanyasaji (wa kingono na kiakili), na kuhakikisha usalama wa watoto.

Tunatoa wito wa mabadiliko ya wazi na ya kimfumo katika sera na mazoea yetu, katika utawala wetu, kila mahali na kila wakati tunapokutana ana kwa ana na kwa pamoja ndani ya ushirika.

Tunapoelekea kwenye Mkutano wa 11, kamati kuu ya WCC, inayokutana Geneva, Uswisi, tarehe 15-18 Juni 2022, kwa hiyo:

Inatoa wito kwa makanisa wanachama wa WCC na washirika wa kiekumene kulaani au kurudia tena kulaani unyanyasaji wa kingono na kijinsia na aina yoyote ya unyanyasaji dhidi ya wanawake, watoto na watu walio katika mazingira magumu; kutangaza kukataliwa kwa hadhi sawa ya watu wote na ukatili huo kama dhambi; na kutekeleza miongozo ya kuzuia unyonyaji wa kingono, unyanyasaji na ukatili.

Inawahimiza sana sekretarieti ya WCC, makanisa wanachama na washirika wa kiekumene kuanzisha na/au kuimarisha sera na mazoea ambayo hutoa msaada kwa watu ambao wananyanyaswa, kuhakikisha uchunguzi kamili, huru na usio na upendeleo, na kuwawajibisha wahusika kwa tabia zao kwa kiwango kamili cha sheria.

Inayaalika makanisa wanachama wa WCC na washirika wa kiekumeni kuongeza juhudi za kitheolojia, kielimu na kujenga uwezo wa kupinga kutengwa kwa wanawake, watoto na watu walio katika mazingira hatarishi, na kujenga ufahamu wa mahusiano sahihi na michakato ya kufuata wakati unyanyasaji, unyonyaji na ukatili unatokea.

Inakaribisha mpango wa kaimu katibu mkuu wa kuendeleza Kanuni za Maadili ili kuzuia na kushughulikia unyanyasaji wa kingono, unyanyasaji na ukatili kwa Mkutano wa11 na mikusanyiko ya baadaye ya WCC.

 


[1] (maelezo kutoka kwenye Tamko la Kamati Kuu ya WC kuhusu Ukatili wa Kingono na Jinsia na Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2018, Novemba 2018)

[2] WCC mnamo mwaka 2011 ilichapisha Wachungaji Wanapokula Kondoo Wao kwa kushirikiana na Shirikisho la Wanafunzi wa Kikristo Duniani kama jibu la ukatili wa kijinsia miongoni mwa makasisi.