Image
Dk. Agnes Abuom. Picha: Peter Williams/WCC

Dk. Agnes Abuom. Picha: Peter Williams/WCC

Dk. Agnes Abuom, kutoka katika kanisa la Angalikana nchini Kenya, ni msimamizi wa kamati kuu ya Baraza la Makanisa Duniani (WCC). Yeye pia ndiye aliyeandika utangulizi katika kitabu kitakachotumika katika Mkutano wa WCC kuhusu Umisheni na Uinjilisti Duniani (CWME). Maelezo hapa chini, yanamuonesha Dk. Abuom akiwa katika mahojiano yanayogusia mambo mbali mbali kuhusu umuhimu wa kihistoria na maudhui ya mkutano huu wa CWME, ambao utafanyika  Arusha, Tanzania mwezi Machi, tarehe 8-13.

Swali: Je unaweza kutueleza kwa kifupi  kuhusu historia ya  CWME?

Dk. Abuom: Sijui kama mnafahamu kuwa tafiti mbalimbali kuhusu asili ya dini zinaonesha kwamba Afrika na sehemu nyingine za ulimwengu wa tatu ndizo kiini kikuu cha ukristo? Afrika ndilo lilikuwa bara la kwanza kabisa kuwa mwenyeji wa mkutano wa umisheni na uinjilisti duniani miaka  60 iliyopita huko  Achimota nchini Ghana, mwaka 1958. Ghana ilipata uhuru wake mwaka mmoja kabla ya mkutano huo. Katika kipindi hicho nchi nyingi za Afrika zilikuwa bado zipo katika harakati za kupigania uhuru kutoka katika tawala za kikoloni. Kwa hiyo, kadri kanisa la Afrika lilivyokuwa likikua kupitia huduma na shughuli za umishenari, bara hili lishuhudia mwanga mpya wa matumaini katikati ya makovu ya majeraha, migawanyiko, kusambaratika kwa jamii, na uwepo wa mifumo ya ukandamizaji ya maisha kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Swali: Kwa nini unaamini kuwa mkutano wa CWME wa mwaka 2018 una umuhimu wa kipekee kihistoria?

Dk. Abuom: Kufanyia mkutano huu Afrika kunatoa fursa ya kujikita katika ukweli na hali halisi ya sasa ya mambo katika bara la Afrika kama vile maumivu, hasira,  pamoja na changamoto mbalimbali zinazohusiana na utumishi wa kiimani katika wakati wa sasa. Mikutano mingine iliyopita ya CWME imekuwa ikishughulikia mambo mbali mbali ya nyakati hizo, kama vile mahusiano ya kimataifa, amani, na mafungamano katika uponyaji na upatanisho. Wakati huu Bara la Afrika linahitaji kutafakari upya na kupima misingi yake ya imani katika kristo na kujiuliza iwapo aina ya ufuasi wa kristo iliyopo inao uwezo wa kufanya uwezeshaji na ubadilishaji wa maisha ya watu duniani, au iwapo inaendeleza ukandamizaji kwa wengine.

Swali: Ni kwa sababu gani mnafanya mkutano huu hapa Afrika?

Dk. Abuom: Mahali hapa tulipopachagua ni muhimu kwa ajili ukumbusho wa sehemu inayofanya kutaniko kati ya imani tofauti tofauti zilizopo katika bara la Afrika: Ukristo, uislamu, na dini za asilia za Afrika. Ni mahali ambapo panahuisha roho ya ukinzani  na simulizi kuhusiana na maono ya kuwa na dunia mbadala, ambayo ina mifumo ya kisiasa na ya kiuchumi ambayo ni rafiki kwa binadamu na kwa dunia kwa ujumla, ambayo imejawa na maadili ya kiroho na kujitoa sadaka. Ukiachilia mbali suala la uongozi, mchango wa kipekee kabisa wa Afrika unabaki kuwa ni ule unaohusu uzoefu na simulizi zinazohusu falsafa ya “ubuntu” au “utu” ambayo inathibitisha kuwepo kwa taswira ya Mungu kwa kila mwanadamu, bila kujali jinsi, kabila, na utaifa; ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha na kuwakaribisha wengine katika utamaduni huu wa ukarimu wa kibinadamu.

Swali: Mambo gani ambayo unaona kuwa ni changamoto zinatotukabili?

Dk. Abuom: Wakati ambapo sisi tunathibisha kuwa ni mawakala tulioitwa na Kristo katikati ya migogoro mikubwa na midogo; biashara ya binadamu na uhamisho wa kulazimishwa; ubaguzi wa rangi na woga wa watu wanaotoka nchi nyingine, ikichanganyika na umaskini wa kupindukia, tunakumbushwa na kupewa changamoto kujitafakari upya

na kujitathmini kuhusu aina ya wito tulioitiwa na dhana nzima ya uanafunzi wa Kristo

ili hatimaye maelezo kuhusu bara letu yalenge kuwa na Afrika iliyo bora, yenye amani, utulivu, heshima na usawa.

Swali: Je Unaweza ukatafakari kwa ufupi maudhui ya mkutano wa Arusha, “Kuenenda katika Roho: wito wa kuwa wafuasi wa mabadiliko?"

Dk. Abuom: Maudhui hii inaendana na matarajio ya sasa ya juhudi mbalimbali za dhati za kulikomboa na kuliweka huru bara la Afrika na dunia kwa ujumla. Ufuasi wa Kristo wenye uwezo wa kubadilisha ni jambo muhimu katika kuhuisha dhana na vitendo vyetu kama wafuasi  ambao tunatangaza habari njema zinazohusiana na njia, miundo na mifumo ya ustawishaji maisha, uimalishaji maisha, na uendelezaji maisha. Kwa hiyo basi, Ufuasi wa kristo wenye uwezo wa kubadilisha katika karne hii ya 21 unahusu kuwakaribisha watu kueleza kuhusu maisha yao na kuwakaribisha wengine kusikiliza, kusikia, na kufanyia kazi kwa pamoja maelezo kuhusu maisha ya kiroho, na maelezo kuhusu mapambano kwa ajili ya kupigania haki, utu na heshima ya binadamu.

Elewa zaidi kuhusu Mkutano wa Umisheni na Uinjilisti Dunani